|
Swahili Poems
I love poetry! I'm very much fascinated by the way poets express their
inner feelings through poetry. I love the rhythm, the depth, and the
power of poetry.
If you love poetry then please read below some Swahili poems
authored by myself and other Swahili poets.
Kitandawili Natowa
Date: July 1, 2000
Author: Hashil S. Hashil, Denmark.
- Natowa kitandawili / mwenye jawabu kutowa
Wako watu sura mbili / majaraha yasopowa
Kuchupa kwao kuwili / nyoyo zao zaunguwa
Watakayo ni muhali / milele hayatokuwa.
- Akili zao ni ghali / kutu zinawasumbuwa
Wapigana na makali / mwenye fani hupekuwa
Warejea ya awali / hawavuki zao puwa
Wala hawana muhali / wamegeuka viluwa.
- Wanapeta pili pili / ungó wao chandaruwa
Upungufu wa akili / ukweli kuutambuwa
Wasemavyo waawali / wengine wajisumbuwa
Hatari yawakabili / kuviwasha vilopowa.
- Mkahawa sihoteli / kushindana kutambuwa
Dibeti zisoukweli / mtuno wakitumbuwa
Kisu kutiwa makali / mwerevu anang´amuwa
Ukweli muukubali / mwiko mwenziwe upawa.
Kitandawili (Jibu)
Date: July 1, 2000
Author: Hassan O. Ali, Ottawa, Canada.
- Watu wenye sura mbili, unao wasimulia
Si watu ni makubeli, wako tayari kuua
Tukae nao kwa mbali, roho wasije zitoa
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.
- Wasifu wao tumbili, kila mti wachupia
Vipando vyetu halali, haweshi kuvivamia
Tena wafanya kejeli, majumbani waingia
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.
- Hawajali hawabali, wendekeza ya dunia
Nyoyo zao za jabali, imani 'mewapotea
Wanajikumbizia mali, nundu zao za ngamia
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.
- Asiyemcha Jalali, Muumba wetu Jalia
Hafai hastahili, kuwaongoza raia
Isiwe mara ya pili, fursa kumuachia
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.
- Beti tano ni kamili, kuongeza sina nia
Kwa chako kitendawili, jibu nimekutolea
Nambie ewe Hashili, kama nimekipatia
Watu wasio murua, ni maadui wa kweli.
Pakacha Pakachuka
Date: May 24, 2002
Author: Hassan O. Ali, Ottawa, Canada.
- Pakacha waniweka, roho juu
Pakacha kila mwaka, hata huu!
Pakacha wanitaka, niwe zuu?
Pakacha pakachuka, chini puu!
- Pakacha nadhikika, dhiki kuu!
Pakacha ninanuka, na kupuu
Pakacha wanicheka, sana tuu!
Pakacha pakachuka, chini puu!
- Pakacha umeruka, kichuguu
Pakacha hujavuka, lima kuu
Pakacha 'tachauka, chau chau
Pakacha pakachuka, chini puu!
- Pakacha sina shaka, si kifuu
Pakacha asotaka, la mkuu
Pakacha huvunjika, lake guu
Pakacha pakachuka, chini puu!
Pakacha Pakachuka ... (jibu)
Date: May 24, 2002
Author: Bakari A. Ali, Reading, U.K.
- Tungo ni safi nzuri, ahsantuu
Utunzi huna dosari, wewe juu
Waenda njema safari, ya majuu
Hassani wewe hodari, ni mkuu
- Beti zanukia wazi, karafuu
Twafurahia ujuzi, ulio juu
Furaha kubwa azizi, sikukuu
Mkono wenye pongezi, shika huu
Pakacha Pakachuka ... (jibu)
Date: May 24, 2002
Author: Hashil S. Hashil, Denmark.
- Pakacha parachuka, wajikuta chini juu
Pakacha lakucheka, mzegazeka nafuu
Pakacha kusarifika, zambarau sio fuu
Pakacha towa talaka, ndio siri ya kifuu
- Pakacha ni kichaka, cha mbuni vitu kuviacha wazi
Pakacha mashaka, wengi wauza mbaazi
Pakacha kushilanga muafaka, shabaha kupanda ngazi
Pakacha kuliamini ni shaka, lageuka utelezi
- Pakacha nakunasihi, fujo zako kuziacha
Pakacha huzimi wala huwashi, wajijua umechacha
Pakacha kipimo chako ni pishi,wengine watoto pacha
Pakacha ubani wako mafushi, mara nyengine mchicha
- Pakacha kujihashuwa uwache, mara hii utadunda
Pakacha makarara kwako cheche, mnyama wako ni punda
pakacha gari lako ni mkweche, wapakia vilovunda
Pakacha miye si cheche, ni sungura kwenye sanda.
Pakacha Pakachuka ... (jibu)
Date: May 25, 2002
Author: Ally bin Aboubakar, London, U.K.
- Wallahi nafurahika, ushairi kuushika,
Malumbano kuyateka, na nyoyo kuburudika,
Ila Pakacha nateta, jawabu hatujalipata,
Pakacha hili nlipi, la Canada au Pemba?
- Dr.nakukumbusha,pakacha la kwenu Pemba,
Muhogo na wake pweza,jioni utajitweka,
Masheli ya kupwaza,si haba utajitwika,
Pakacha hili nlipi,mbona hwelitaja?
- Karafuu hichumia, na mpeta kuokotea,
Leo mbona mwalinunia, pakacha hili la kujivunia,
Wallahi najivunia, mipesa nejichumia,
Dr.Hassan hebu nambia, kabla sijakufokea,
- Komputa hutaitia, ndani ya pakacha nakwambia,
Ila ndio tweanzia, karafuu na kijio kutafutia,
Hebu leo twambie, huko canada lipo hilo Pakacha
Au nlile la aslia , Pemba na Unguja lanukia?
N'na Paka Guniani
Date: October 25, 2000
Author: Hassan O. Ali
- Sitathubutu kusema, nimeshakula yamini
Mchota maji kisima, hata iwe muadhini
Hatanitoa kalima, wala hatanizaini
N'na paka guniani, sitathubutu kusema
- Paka huyu kisirani, si paka ni ngawa-nyumba
Avuua kaangoni, mara akinusa vumba
Jeleko la kizamani, alitipa kama pamba
N'na paka guniani, sitathubutu kusema
- Si paka ni subiani, jini amepigwa chapa
Usipokaa makini, mara hukwendesha kapa
Ndio hasema sineni, kanishinda namtupa
N'na paka guniani, sitathubutu kusema
- Sitasema akarudi, akazidi kunitimba
Nimeifanya juhudi, mwituni nenda msumba
Hutendwa lisilo budi, mdomo ninaufumba
N'na paka guniani, sitathubutu kusema
Heko Kwa Bwana Hassani ... (jibu)
Date: October 25, 2000
Author: Ahmed Rashid
- Japo paka subiani, shetani wa ujinini,
Sasa yuko hatarini, simtoe guniani,
Enenda naye porini, umfukie shimoni,
Heko kwa Bwana Hassani, kalitupe paka shume.
- Kalitupe paka shume, likatoweke mwituni,
Litupe lisisimame, limetuchosha nyoyoni,
Uhakika tuuseme, ni paka shume ja nyani,
Heko kwa Bwana Hassani, kalitupe paka shume.
- Paka hili jizi sana, masinzi tele usoni,
Mbinuze ni nyingi sana, kuiba nyama jikoni.
Hata Hassani kinena, shume harudi nyumbani,
Sema siogope shume, shume harudi nyumbani.
- Kusema usiogope, yanene yote wavuni,
Na changa moto tukupe, uyatoe ya moyoni,
Kwa pamoja tulitupe, shume lilo guniani,
Heko kwa Bwana Hassani, kalitupe paka shume.
|